Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Monday, April 29, 2013

KIPINDI CHA TELEVISION CHASAIDIA KUTATUA KERO ZA WAZEE KAGERA



picha za wazee wakiwa wamepiga pozi picha kwa hisani ya mtandao

Na mwandishi wetu
Bukoba
 
Kipindi cha Television kilichoonesha adha na matatizo ya wazee wa kituo cha Kilima kilichopo mkoani Kagera kimeleta faraja kwa wazee hao baada ya wafadhili kutoka nchini Marekani kuamua kusaidia kituo hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwemo kufuta ratiba ya mlo mmoja kwa siku na kukarabati mabweni ya kituo hicho.
 
Kipindi hicho kilirushwa na Television ya Channel ten kupitia kipindi cha kila wiki cha 'Barua kutoka kanda ya ziwa' na kuingizwa katika mtandao wa internet wa Youtube ambapo shirika la kimataifa la UKIMWI Orphans Assistance (UOA) la nchini Marekani lenye tawi lake hapa nchini liliamua kuwasiliana na serikali ya mkoa wa Kagera pamoja na shirika la Saidia Jamii ya wazee Kagera (SAJAWAKA) kuhusu adhima yao ya kusaidia wazee hao.
 
Akiongea mara baada ya kutiliana saini katika Mkataba wa Maelewano baina ya serikali na mashirika hayo Mratibu wa SAJAWAKA ambaye pia ni msimamizi wa mradi wa kusaidia kituo hicho Bw Emmanuel Rugeiyamu ameshukuru mchango wa vyombo vya habari nchini Tanzania kwa kusaidia jamii hasa watu wanaoisshi maeneo ya vijijini.
 
"Kama waandaaji wa kipindi hicho wasingefika katika kituo hicho nani angejua matatizo ya wazee hawa, kwakweli kipindi hiki kimewaokoa wazee" alisema Rugeiyamu na kuongeza kwamba " katika kipindi cha miaka mitano UOA kwa kushirikiana na SAJAWAKA tutaboreshewa mazingira ya kituo kwa kuweka huduma huduma zote wanazostahili kupata wazee katika umri wa uzee na watoto yatima walioko hapo pamoja na kuwapatia mlo kamili wa usiku na mchana"
 
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa Kagera Bw. Nassor Mnambila aliyeesaini mkataba huo kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwasababu kituo hicho kipo chini ya wizara hiyo, alisema kuwa serikali ya mkoa wa Kagera imehusika kusaini mkataba wa maelewano kwa ajilia ya ufuatiliaji wa karibu katika kituo hicho na kwamba katika makubaliano hayo UOA na SAJAWAKA yatahusika na kukarabati miundombinu ya kituo ikiwemo mabweni, bafu, nyumba za watumishi, jiko, stoo na bwalo la chakula na kuweka samani ndani ya majengo hayo.
 
"serikali itaendelea kuhakikisha utulivu na amani katika kituo hicho na itaendelea kutoa huduma zilizokuwa zikitolewa hapo mwanzo kama mishahara ya watumishi wa kituo hicho na huduma nyingine kama chakula ilizokuwa ikizitoa tangu awali." alisema.
 
Akiongea na waandishi wa Habari mwandaaji wa kipindi hicho cha "Barua kutoka kanda ya Ziwa" Bw Mathias Byabato alisema kwamba pamoja na mchango unaotolewa na waandishi wa habari katika mkoa wa kagera lakini serikali ya mkoa huo hauthamini.
 
"Unajua tulipokwenda kurekodi wazee hawa wa Kilima tulizuiwa kupiga picha lakini tulipiga picha kwa siri, ndiyo maana kwa waliokiona picha hazikuwa bora, lakini tumerusha kipindi kwenye TV kisha kukiweka katika mitandao ya kijamii wamejitokeza wafadhili kutoka nje ya nchi lakini serikali ya mkoa haitoi hata shkurani kwetu wala kuboresha mazingira ya kituo mapaka wasubiri misaada" alisema Byabato na kuongeza
 
" hatukuonesha matatizo ya wazee kwa lengo la kuwarika walioko nje ya nchi,tulitaka serikali itimize wajibu wake na isisubiri wafadhili kutatua matatizo yaliyomo katika uwezo,sera na mipango yake ya kuwasaidia wananchi wake na mazoea kwamba suruhisho la matatizo katika jamii ni kupata ufadhili badala ya kutegemesa rasilimali za nchi" alisema.
 
Kituo cha kutunza wazee wasiojiweza na yatima cha Kiilima kipo katika wilaya ya Bukoba vijijini na kilianzishwa mwaka 1972 na serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambapo kwa sasa kinao wazee zaidi ya 50.
 
mwisho

No comments:

Post a Comment