Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Thursday, August 2, 2012

WADAU WAIBEBESHA LAWAMA HALMASHAURI MULEBA

Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari wakikimbia na magunia katika mbio za mita 100 wakati wa tamasha la wanachama wa klabu za kupinga rushwa.

 Na Livinus Feruzi
Muleba

WADAU wa elimu halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameinyoshea kidole halmashauri hiyo kuhusika na kushuka kwa kiwango cha elimu kila mwaka, kutokana na kudaiwa kuwepo kwa ushirikano hafifu baina walimu na idara ya elimu.

Wakichangia mada wakati wa mdahalo wa elimu ulioandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Kagera (Kangonet) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil societies kwa ajili ya kuangalia sababu za kushuka kwa kiwango cha elimu na kuzipati ufumbuzi, wadau hao walisema uhusiano hafifu kati ya idara ya elimu na walimu kumepelekea walimu kukosa ari na mwamko wa kutekeleza wajibu wao.

Mmoja wa wadau hao Bw. Christoph Lucas alisema idara ya elimu kupitia kwa maafisa wake wamejisahau, ambapo alidai hawathamini walimu hasa wanapohitaji msaada kutoka kwenye ofisi zao na kuwa hali hiyo inapelekea walimu kukata tamaa hivyo kutofanya kazi zao ipasavyo.


 Naye Bw. Rainford Mujuni alidai tatizo la kila mwaka elimu kushuka linatokana dharau za maafisa elimu wanazozionyesha kwa walimu huku akiwatuhumu kukaa ofisi kama mabosi huku wakishidwa kutembelea shule na kuzifanyia ukaguzi. “Kiukweli kushuka kwa elimu katika wilaya yetu afisa elimu hawezi kukwepa lawama maana anachokifanya yeye ni kukaa ofisi kama bosi na kudharua walimu, kwa hali hii haiwezekani mwalimu akawa na ari ya kufanya kazi ipasavyo” aliongeza Mujuni

Mdau mwingine wa elimu Bw. Ayuob Kiiza alisema kutokana na uhusiano huo hafifu baina ya walimu na idara ya elimu imepelekea baadhi ya wakuu wa shule kuogopa kuingia katika ofisi hizo na hivyo kupelekea taarifa muhimu kushindwa kupatikana.

Ni kutokana na hali hiyo wadau hao wameitaka halmashauri kuondoa kasoro zilizobainishwa ili kuongeza kiwango cha ufaulu ambacho kilianza kushuka tangu mwaka 2008, ambapo takwimu za mkoa zinaonyesha kuwa mwaka 2008 katika matokeo ya darasa la saba halmashauri hiyo ilishika nafasi ya tatu, 2009 nafasi ya tano, 2010 nafasi ya sita huku mwaka 2011 ikishika nafasi ya saba ikiwa ni ya pili kutoka mwisho.

 Kwa upande wa afisa elimu taaluma wa shule za sekondari wilayani humo Bi. Doris Bitegeko na afisa elimu taaluma wa shule za msingi Bw. Bukuru Malembo kwa pamoja wamekiri kuwepo kwa kasoro kadhaa na kuhaidi kuzishugulikia ili kuleta wa elimu katika wilaya hiyo.

 “Sisi kama idara ya elimu wamechukua kasoro hizo tunahaidi kuzishughulikia maana hata sisi tunaumia hakuna mtu anayependa hali ya elimu iwe kama ilivyo nawahakikishia tutajitahidi kuondoa doa hili la kushuka kwa elimu” aliongeza Bw. Bukuru Malembo afisa elimu taaluma wa shule za msingi.

 Hata hivyo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mradi wa utafiti wa elimu Tanzania wa UWEZO ambao ulifanyika mwaka 2011 katika wilaya 132 za Tanzania Muleba ilishika nafasi ya 103, ambapo kwa kutumia mitaa la darasa la pili ni asilimia 77 ya wanafunzi wa darasa saba waliofanya vizuri katika somo la kiswahili. Mwisho

No comments:

Post a Comment