Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Wednesday, December 5, 2012

WAKULIMA NA WAFUGAJI WA SAMAKI BUKOBA WAILILIA SERIKALI





Wafugaji wa samaki kutoka kata tatu za halamshauri ya weilaya ya Bukoba wakifuatilia mafunzo juu ya ufugaji bora wa wa samaki ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wao kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hiyo.

Bi. Rehema akiwafundisha wafugaji jinsi ya kutengeneza mabwawa na kupandiza idadi inayofaa kwa kila bwawa

Bw. Peter Meshashua afisa kilimo kutoka halamshauri ya wilaya ya Bukoba akitoa mada wakati wa mafunzo ya wakulima yaliyofanyika Kemondo
Na Livinus Feruzi
Bukoba

WAFUGAJI wa samaki katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoa wa Kagera wameiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwatafutia soko la samaki wao ili kuwezesha wafugaji kutumia sekta ya kilimo na ufugaji kujikwamua kiuchumi.

Wafugaji hao walitoa ombi hilo juzi katika kata ya Kemondo Bukoba vijijini mara baada ya mafunzo yaliyokuwa yanatolewa kwa wawakilishi wa vikundi vya ufugaji wa samaki kwa kutumia mabwawa, kutoka kwenye kata tatu za halmashauri hiyo.

Mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na halmashauri ya wilaya ya Bukoba kwa kushirikiana na asasi za kiraia mkoa wa Kagera (Kangonet) chini ya ufadhili wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa( UNDP) yanalenga kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya milenia kupitia sekta ya kilimo MAF.

Mmoja wa wafugaji hao Bw. Theogenes Rumboyo na Justian Modest kutoka kikundi cha Abesiga wanasema Machi 2 mwaka huu watu kumi walijikusanya pamoja na kuamua kuchimba bwawa na kisha kuchangishana fedha za kununua vifaranga 500 na hivyo kuanzisha ufugaji wa samaki.

Bw. Rumboyo alisema kwa sasa samaki wameishazaliana na tayari ndani ya wiki hii wanatarajia kuvuna samaki hao lakini bado hawajui ni wapi watauza kitoweo hicho muhimu ili walau kurejesha gharama walizotumia tangu kuanzishwa kwa bwawa hilo.

“Tatizo kubwa la ufugaji wa samaki ni kutopatikana kwa masoko mfano kikundi chetu wiki hii tunatarajia kuvuna samaki lakini hatujui tutawauza wapi….Sana sana watu tunaowategemea kuwauzia ni vibandani (wanaonunua kwa ajili ya kitoweo nyumbani ) alisema Bw. Rumboyo

Hata hivyo alisema iwapo soko la kuuza samaki hao litaendelea kuwa gumu watawagawana na kuwatumia nyumbani kama kitoleo, ambapo aliongeza “ tunaomba serikali na mbunge wetu watusaidie kupata masoko ili walau hata kupata gharama zilizokwishatumika” 

Naye Johanes Joel kutoka katika kijiji cha Kanazi alisema pamoja na kikundi chao kwa sasa kuna na vifaranga vya kutosha, bado wameshindwa kuvuna kutokana na kukosa soko la kuviuza.

Alisema iwapo serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo watatilia mkazo suala la ufugaji wa samaki, sekta hiyo ina uwezekano mkubwa wa kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla na hivyo kuwezesha kufikiwa kwa malengo.

Awali mkurugenzi wa shirika la mwangaza wa familia la mjini Bukoba Bw. Innocent Bideberi alisema kwa kutambua tatizo hilo ndio maana katika mradi huu wa MAF wameanzisha vituo vya kupata taarifa za msingi za masoko katika eneo la mradi.

Bw. Bideberi alisema vituo hivyo vitakuwa na vifaa vyote vya mawasiliano na hivyo kuwataka wakulima na wafugaji  kutumia vituo hivyo katika kupata taarifa mbalimbali za masoko ndani na nje ya nchi.

Mwisho

No comments:

Post a Comment