Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Wednesday, April 11, 2012

Matumaini mapya kutoa ruzuku ya milioni 48.4 kwa wajane 200 Kagera

Mratibu wa shirika la kuwezesha watoto yatima na wajane la matumaini mapya Bw. Gosbert Kaserwa akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa akinamama wajane na walezi wa watoto yatima 40 wa awamu ya kwanza kutoka wilaya Bukoba na Missenyi, kulia kwake ni mkuu wa kitengo cha watoto wa shirika hilo Bi. Edina Jacob.







Baadhi ya akinamama wajane na walezi wa watoto yatima wanaohudhuria mafunzo ya siku tano yakupatiwa ruzuku ambayo yameandaliwa na shirika la matumaini mapya, wakifuatilia  maelezo kutoka kwa viongozi wa shirika.




Akinamama wajane na walezi wa watoto yatima kutoka wilaya ya Bukoba na Missenyi wakiomba kwa mungu na kuliombea shirika baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wajane 200 ambao watapatiwa ruzuku kati ya 565 walioomba, kila mjane na mlezi wa watoto yatima watapatiwa shilingi 240,000



Na Mwandishi wetu
Bukoba

SHIRIKA la kuwezesha watoto yatima na wajane katika manispaa ya Bukoba la matumaini mapya linatarajia kutoa ruzuku ya zaidi ya shilingi milioni 48.4 kwa wanawake wajane na walezi wa watoto yatima 200 ili kuwapunguzia ugumu wa maisha unaowakabili.

Mratibu wa shirika hilo Bw. Gosbert Kaserwa alisema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa akinamama wajane na walezi wa watoto yatima 40 wa awamu ya kwanza kutoka wilaya Bukoba na Missenyi.

Alisema kabla ya wanawake hao kupatiwa ruzuku hiyo kwanza shirika linawapatia mafunzo juu ya masuala mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kusimamia na kutetea haki zao, ambapo zaidi ya shilingi milioni 66 zitatumika katika mafunzo hayo.

Bw. Kaserwa alisema zoezi la utoaji wa ruzuku ambalo linaenda sambamba na mafunzo litafanyika kwa awamu tano tofauti, huku kila mwanamke akitarajiwa kupewa kiasi cha shilingi 240,000.

Mratibu huyo aliwataka wanawake hao kutumia fedha hizo za ruzuku katika kuendeleza miradi yao ili ziwasaidie kuboresha maisha yao na familia zao ikiwemo kupata mahitaji muhimu ya kila siku ambayo awali walikuwa wanashindwa kuyapata.

Wakati wa mafunzo hayo ya siku tano mada zipatazo 20 zitafundishwa kwa wanawake hao, ambazo miongoni mwake ni sheria ya ndoa ya mwaka 1971, haki za wajane na watoto yatima, matumizi bora ya raslimali za familia, andiko la mradi ya kijamii na ukatili na unyanyasji wa kijinsia.

Mwisho.



No comments:

Post a Comment