Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Thursday, April 5, 2012

Mwanafunzi aachishwa shule na kisha kuozeshwa


Na Mwandishi wetu 
Bukoba vijijini

MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Maruku Bukoba vijiji Felista Trazias (16) anadaiwa kuozeshwa baada ya kuachishwa shule katika mazingira ya kutatanisha.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Bwizanduru halmashauri ya wilaya ya Bukoba Bw. Edward Mwemezi alisema mwanafunzi huyo aliachishwa shule mwaka jana, na kuajiriwa na mama yake wa kambo kuuza pombe za kienyeji kijijini hapo.

Alisema mwaka jana baada ya kupokea taarifa za mwanafunzi huyo kuachishwa shule na kisha kuajiriwa kuuza pombe za kienyeji, taarifa hizo ziliripotiwa polisi na kupewa RB namba BU/RB/6730/2011 lakini mwanafunzi huyo aliendelea na kazi hiyo.

Bw. Mwemezi alisema binti huyo ambaye alikuwa haishi na wazazi wake, aliendelea kuuza pombe mpaka mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuolewa na mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Bw. Oscar Elias mkazi wa kitongoji cha Maiga kijijini hapo.

Kutokana na suala hilo mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Samwel Kamote ameagiza kukamatwa kwa wahusika wote ambao ni pamoja na binti huyo, mwanaume aliyemuoa, mama wa kambo Bi. Mecktilida Venant na mume wake Bw. Venant Ndyanabo ambao wanadaiwa kushiriki kumuozesha mwanafunzi huyo.

Barua ya mkuu huyo wa wilaya ya Machi 7 mwaka huu kwenda kwa afisa tarafa ya Kyamtwara Bukoba vijijini aliagiza watendaji husika kuomba msaada wa polisi ili kuhakikisha wahusika hao wanne wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo afisa huyo mtendaji alisema kuwa juzi walifanikisha kumkamata mwanafunzi huyo huku watuhumiwa wengine watatu (muoaji na walioshiriki mkuozesha ) wamekimbia, na kuongeza kuwa wanaendelea kutafutwa.

Naye Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Bw. Vitus Mlolore alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kuwa polisi kwa kushirikiana na afisa mtendaji wa kijiji cha Bwizanduru wanaendelea kuwasaka watuhumiwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Kuhusu kukamatwa kwa binti huyo na kisha kuachiwa. Bw. Mlolere alisema kuwa mwanafunzi huyo hawezi kufunguliwa mashtaka kwa madai kwamba yeye ndio mwathirika.

Mwisho

No comments:

Post a Comment