Shamba la migomba ambalo limeathiriwa na ugonjwa unyanjano kupita mradi wa MAF shamba hili likitumika kwa mazao mengine inaweza kusadia kufikiwa kwa malengo ya milenia. |
Na Livinus Feruzi
Bukoba
IKIWA imebaki takribani miaka mitatu kabla ya kuhitimisha
mpango wa malengo ya Milenia 2015, halmashauri ya wilaya ya Bukoba imezindua mradi
wa kuharakisha kufikiwa kwa malengo hayo kupitia sekta ya kilimo.
Mradi huo wa MAF unaotekelezwa kwa kushirikiana asasi
za kiraia mkoa wa Kagera ulizinduliwa jana na mkuu wa wilaya ya Bukoba Bi. Zipporah
Pangani na unalenga kuharakisha kufikiwa kwa lengo la milenia namba moja la kupunguza
umaskini wa kipato na njaa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Bi. Pangani alisema
ili mradi huo uweze kufanikiwa inahitaji wananchi kujituma na viongozi kuwajibika
kwa hali ya juu na kutaka fursa hiyo itumike kuleta mabadiliko.
Alisema kutokana na hali ya hewa kuwa nzuri katika wilaya
hiyo, hakuna sababu ya wananchi kushindwa kujitosheleza kwa chakula na kuwa wakulima
wakipatiwa pembejeo za kilimo inawezekana halmashauri hiyo kufikia malengo ya
milenia.
“Tunataka mabadiliko baada ya mradi huu ni lazima
maisha ya wananchi yabadilike, sioni sababu ya wilaya ya Bukoba yenye hali nzuri
ya hewa kushindwa kuzalisha chakula zaidi” alisema Bi. Pangani.
Mkuu huyo wa wilaya alitaka makundi maalum katika
mradi huo kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha wanaanzisha vikundi vya wakulima wa
zao la alizeti na kuahidi serikali kutoa ushirikiano ili kufanikisha mradi huo.
Awali Mratibu wa mradi huo wa MAF kupitia asasi za
kiraia mkoa wa Kagera Bw. Joas Kaijage alisema unalenga kupunguza njaa na umasikini
wa kipato na kuwapatia wananchi taarifa za masoko, fursa za mikopo na mitaji
Aidha unalenga kuwapatia wakulima taarifa sahihi za
teknologia mbalimbali za kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wake mratibu wa MAF halmashauri ya wilaya
ya Bukoba Bw. Ngabo Pamba mradi umejikita katika kuanzisha mazao ya alizeti,
mihogo na mpunga wa nchi kavu ili yawe mbadala kwa mazao makuu ya kahawa na
migomba.
Nyingine ni kuendeleza ufugaji wa kuku wa kienyeji na ufugaji
wa samaki wa kienyeji.
Mradi huo wa majaribio kwa miezi mitano unafadhiliwa
na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) na unatekelezwa kwa
ushirikiano kati ya halmashauri ya wilaya ya Bukoba na mtandao wa asai zisizo
za kiserikali mkoa wa Kagera (KANGONET).
mwisho
No comments:
Post a Comment