Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Monday, November 26, 2012

KAGASHEKI AZIDI KUIKOROGA CCM BUKOBA MJINI





Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Balozi Khamis Kagasheki akizungumza katika moja ya mkutano
Na Livinus Feruzi
Bukoba

CHAMA cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Bukoba mkoa wa Kagera kimezidi kugawanyika na kuonyesha mgawanyiko huo hadharani, kufuatia mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Balozi Khamis Kagasheki kutangaza rasmi kupingana na maamuzi ya Baraza la madiwani yaliyofikiwa juu ya kuvunjwa kwa soko kuu la mji huo na kulijenga upya.

Hata hivyo kauli ya Balozi Kagasheki kupinga soko hilo kuvunjwa inatofautina na hile aliyoito mwazoni mwa wezi juni katika uwanja wa uhuru mjini Bukoba uliofanyika baada ya baadhi ya wananchi kupinga ujenzi huo, ambapo alisema soko hilo lazima livunjwe ili kujengwa upya kwani limepitwa na wakati.

Jana katika mkutano wa hadhara Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa maliasili na utalii alimshutumu Meya wa manispaa hiyo Dkt. Anathory Amani, madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kwa kile alichodai kwamba wanataka kumburuza katika maamuzi juu ya utendaji wa halmashauri.

Alisema soko hilo halitavunjwa mpaka kupata muafaka wa wafanyabiashara walioko ndani ya soko hilo na kuongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuachwa ili waweze kuamua hatma ya soko hilo.

Aidha aliwatahadharisha viongozi wa CCM wilaya ya Bukoba mjini kwamba mchezo unaoendelea ndani ya chama hicho, huenda jimbo hilo likachukuliwa na chama cha upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kama ilivyotokea wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000.

“2000 jimbo hili lilipotea kutoka mikononi mwa CCM… na sababu ya kupotea ni CCM ambao ndio walilitoa kwa sababu walikuwa na mivurugano na uchu wa madaraka na wapo waliosadia jimbo kwenda upinzani” alisema Balozi Kagasheki.

Aliongeza kuwa “2005 CCM tulijipanga na kuchukua upya jimbo, lakini kwa sasa mchezo ambao umeanza ndani ya CCM huenda jimbo likaelekea uko uko na mimi wakati huo huenda nikawepo au nisiwepo” .

Kwa miezi kadhaa sasa ndani ya CCM wilaya ya Bukoba mjini sio shwari kwani tayari Meya ya manispaa hiyo Dkt. Amani alitishia kujiuzulu wadhifa huo baada ya kuandika barua na kisha kuisambaza kwa viongozi mbalimbali wilaya na mkoa kabla ya kushawishiwa na baadhi ya viongozi kusitisha azma yake.

Hata hivyo mwazoni mwa wiki juzi katika kikao cha baraza la madiwani, ambacho pia kilihudhuriwa na Mbunge huyo kililidhia  kuvunjwa kwa soko hilo, huku meya akitangaza rasmi kuvunjwa ifikapo January 15 mwaka 2013.

Aidha Dkt. Amani alisema maamuzi ya kuvunja soko hilo yako palepale kwani ni utekelezaji wa maamuzi ya vikao halali vya halmashauri ya manispaa ya Bukoba, huku akiugwa mkono wa asilimia kubwa ya madiwani na wananchi wa kawaida.

Mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Bw. Khamis Kaputa akitoa ufafanuzi wa mradi huo wakati wa baraza hilo alisema maandalizi na taratibu zote za kuvunja soko hilo zinaendelea vizuri, ikiwa ni pamoja na kuandaa mazingira ya kuhamishia wafanyabishara walioko katika soko hilo.

Hata katibu wa CCM mkoa wa Kagera Bw Evelin Mushi ambaye alihudhuria mkutano huo ingawa alishuhudiwa bila kukaa meza kuu, alipohojiwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi wa mgogoro ndani ya chama hicho alisema hawezi kutoa ufafanuzi wowote kwani hakuhudhuria mkutano huo.

“siwezi kuzungumza chochote kwa sababu sijahudhuria mkutano huo na kama unahitaji ufafanuzi kesho njoo ofisini ” aliongeza Bw. Mushi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya mkutano huo alisema tofauti za viongozi hao ndani CCM hazikutakiwa kuwekwa wazi mbele ya wananchi hususani katika suala maendeleo.

Hata hivyo wakati meya huyo akishambuliwa na mbunge, alikuwa amekaa katika jukwaa kuu na kutulia mithili ya kwamba hasikii kinachozungumzwa na baada ya mkutano kufungwa aliondoka huku akicheza mziki wa chama hicho.

 Takribani shilingi bilioni 12 zinatarajiwa kutumika kujenga soko hilo ambalo linatarajiwa kuwa la kisasa zaidi.

No comments:

Post a Comment