Miongoni mwa nyumba zilizoezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali katika kata ya Buhembe nje kidogo ya mji wa Bukoba. |
Na mwandishi wetu
Bukoba
NYUMBA zilizoezuliwa na
mvua iliyoambatana na upepo mkali (Oktoba 25) katika manispaa ya Bukoba
zimeongezeka kutoka nyumba 25 hadi kufikia nyumba 93 na kupelekea wananchi 436 kuachwa
bila makazi.
Mvua hiyo iliyonyesha jana
asubuhi kwa takribani nusu saa ilipelekea kuezuliwa kwa nyumba hizo, huku
baadhi yake kubomoka kwenye kata tatu za Buhembe, Kahororo na Nyanga, ambapo
pia imeharibu mazao mbalimbali na kusababisha hofu ya njaa kwa wananchi husika.
Diwani wa kata ya Buhembe Bw. Alexander Ngalinda alisema
kuwa katika kata yake nyumba 68 zimeezuliwa na kusababisha wananchi
wanaokadiriwa kufikia 340 kukosa mahala pa kuishi.
Bw. Ngalinda alitaja mazao
yaliyoharibiwa na mvua hizo kuwa ni pamoja na mahindi, maharage, migomba na
marando, ambapo tathimini ya hasara iliyosababishwa na maafa hayo bado inaendelea
kufanyika.
Katika Kata ya Nyanga
nyumba 15 zimeezuliwa na baadhi yake kubomoka ambapo wananchi wanaokadiriwa
kufikia 60 wamalazimika kulala kwa majirani baada ya kukosa mahali pa kulala .
Naye Diwani
wa kata ya Nyanga Bw. Deusdedith Mtakyahwa alisema kuwa bado wanaendelea
kutembelea maeneo yote ya kata hiyo ili kubaini athari nyingine zilizotokana na
mvua hizo.
Mwenyekiti
wa mtaa wa Bunukangoma uliopo kata Kahororo, ambayo ni kata nyingine
iliyoathiriwa na mvua hizo Bw, Cosmas Rwabigene alisema kuwa katika mtaa wake
wananchi 36 hawana makazi kufuatia nyumba zao kumi kuathiriwa na mvua hizo.
Wananchi katika kata hizo
zilizoathirika wameomba serikali na wadau wengine kuwasaidia fedha za kununulia
mabati na kujengea nyumba zao na ikiwa ni pamoja na kupatiwa chakula kufuatia
mazao waliyoyategemea kuharibika.
Mkuu wa mkoa wa Kagera
kanali mstaafu Fabian Massawe ameanza ziara rasmi katika kata zilizoathirika
ili kujionea hali halisi na tathmini ya harasa iliyosababishwa na mvua hizo
itatolewa baadae.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment