Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Thursday, September 27, 2012

MANISPAA YATAKIWA KUTUMIA WALIMU WA BINAFSI

MWANDISHI WETU
BUKOBA


HALMASHAURI ya manispaa ya Bukoba kupitia idara ya elimu imetakiwa kuanzisha utaratibu wa kutumia walimu wa shule binafsi wakati wa kuandaa majibu ya mitihani ya majaribio ya wilaya (mock) kabla ya kuisahihisha ili kuondoa mkanganyiko wa majibu na kuleta tafsiri sahihi ya mitihani hiyo. 


Wito huo umetolewa juzi mjini Bukoba na meneja wa shule za Kaizilege zinazofundisha kwa michepuo ya Kiingereza (KEMEBOS) Bw.Eulogius Katiti wakati wakizungumza na wazazi, walezi na wanafunzi katika mahafali ya tatu ya wahitimu wa darasa la saba.


Alisema katika mitihani ya majarobio na kujipima uwezo (Mock ) baadhi ya maswali hususan ya kuchagua wakati mwingine yanaletwa na majibu yasiyo sahihi na hivyo kuleta shida na hata kupelekea wanafunzi kushindwa kutoa jibu sahihi licha ya kufahamu jibu lake.


Bw. Katiti alisema hali hiyo inapelekea mitihani hiyo kupewa tafsiri isiyo sahihi na kuongeza kuwa kwa kutambua madhara ya tatizo hilo tayari wamechukua uamuzi wa kuonana na afisa elimu wa manispaa hiyo ili kumweleza jinsi ya kuliondoa.


“Tatizo hili linaleta shida hata kwa wanafunzi kushindwa kutoa jibu lililosahihi kutokana na wakati mwingine maswali ya kuchagua kukosa jibu, tayari tumechukua hatua za kumuona afisa elimu ili waanzishe utaratibu wa kutumia walimu wa shule binafsi kuandaa majibu sahihi (marking guide) kabla ya zoezi la kusahihisha kuanza” alisema meneja huyo. 


Aidha aliongeza kuwa halmashauri hiyo pia inatakiwa kutumia walimu hao hata wakati wa zoezi la utungaji wa mitihani ili kuepuka kuleta maswali yasiyokuwa na maana halisi inayokuwa imetarajiwa. 


Awali Mwenyekiti wa kamati ya shule hizo Bw. Abubakhari Kagasheki aliwataka wazazi na walezi kujenga tabia ya kutembelea wao shuleni ili kufuatilia maendeleo yao, ikiwemo kutoa ushauri kwa viongozi wa shule jinsi ya kuendelea kuboresha taaluma. Mwisho

No comments:

Post a Comment