Na Mwandishi wetu
Bukoba
SHIRIKA la kuwezesha watoto yatima na
wajane katika manispaa ya Bukoba la matumaini mapya linatarajia kutoa ruzuku ya
zaidi ya shilingi milioni 48.4 kwa wanawake wajane na walezi wa watoto yatima 200
ili kuwapunguzia ugumu wa maisha unaowakabili.
Mratibu wa shirika hilo Bw. Gosbert Kaserwa alisema hayo jana
wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa akinamama wajane na walezi wa watoto
yatima 40 wa awamu ya kwanza kutoka wilaya Bukoba na Missenyi.
Alisema kabla ya wanawake hao kupatiwa
ruzuku hiyo kwanza shirika linawapatia mafunzo juu ya masuala mbalimbali ili
kuwajengea uwezo wa kusimamia na kutetea haki zao, ambapo zaidi ya shilingi milioni
66 zitatumika katika mafunzo hayo.
Bw. Kaserwa alisema zoezi la utoaji wa
ruzuku ambalo linaenda sambamba na mafunzo litafanyika kwa awamu tano tofauti,
huku kila mwanamke akitarajiwa kupewa kiasi cha shilingi 240,000.
Mratibu huyo aliwataka wanawake hao kutumia
fedha hizo za ruzuku katika kuendeleza miradi yao
ili ziwasaidie kuboresha maisha yao
na familia zao ikiwemo kupata mahitaji muhimu ya kila siku ambayo awali
walikuwa wanashindwa kuyapata.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment