Na Mwandishi wetu
Bukoba vijijini
MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule ya
sekondari ya Maruku Bukoba vijiji Felista Trazias (16) anadaiwa kuozeshwa baada
ya kuachishwa shule katika mazingira ya kutatanisha.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Bwizanduru halmashauri ya
wilaya ya Bukoba Bw. Edward Mwemezi alisema mwanafunzi huyo aliachishwa shule
mwaka jana, na kuajiriwa na mama yake wa kambo kuuza pombe za kienyeji kijijini
hapo.
Alisema mwaka jana baada ya kupokea taarifa za
mwanafunzi huyo kuachishwa shule na kisha kuajiriwa kuuza pombe za kienyeji,
taarifa hizo ziliripotiwa polisi na kupewa RB namba BU/RB/6730/2011 lakini
mwanafunzi huyo aliendelea na kazi hiyo.
Bw. Mwemezi alisema binti huyo ambaye alikuwa haishi
na wazazi wake, aliendelea kuuza pombe mpaka mwanzoni mwa mwaka huu baada ya
kuolewa na mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Bw. Oscar Elias mkazi wa
kitongoji cha Maiga kijijini hapo.
Kutokana na suala hilo mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw.
Samwel Kamote ameagiza kukamatwa kwa wahusika wote ambao ni pamoja na binti
huyo, mwanaume aliyemuoa, mama wa kambo Bi. Mecktilida Venant na mume wake Bw.
Venant Ndyanabo ambao wanadaiwa kushiriki kumuozesha mwanafunzi huyo.
Barua ya mkuu huyo wa wilaya ya Machi 7 mwaka huu
kwenda kwa afisa tarafa ya Kyamtwara Bukoba vijijini aliagiza watendaji husika kuomba
msaada wa polisi ili kuhakikisha wahusika hao wanne wanakamatwa na kufunguliwa
mashtaka kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo afisa huyo mtendaji alisema kuwa juzi
walifanikisha kumkamata mwanafunzi huyo huku watuhumiwa wengine watatu (muoaji
na walioshiriki mkuozesha ) wamekimbia, na kuongeza kuwa wanaendelea kutafutwa.
Naye Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Bw. Vitus
Mlolore alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kuwa polisi kwa kushirikiana na
afisa mtendaji wa kijiji cha Bwizanduru wanaendelea kuwasaka watuhumiwa ili
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Kuhusu kukamatwa kwa binti huyo na kisha kuachiwa. Bw.
Mlolere alisema kuwa mwanafunzi huyo hawezi kufunguliwa mashtaka kwa madai
kwamba yeye ndio mwathirika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment