Mwenyekiti wa bodi ya chama cha ushirika mkoa wa Kagera KCU Bw. John Binushu akifungua mkutano mkuu wa chama hicho, mkutano huu ndio ulitangaza bei ya kahawa kwa msimu huu |
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu, ambao ndio wawakilishi wa wakulima wakifuatilia mkutano ambao ulitangaza bei ya kahawa |
Na Livinus Feruzi
Bukoba
WAKULIMA wa
zao la kahawa mkoa wa Kagera wamepinga vikali kitendo cha chama kikuu cha
ushirika mkoa wa Kagera (KCU 1990 LTD) kushusha bei ya zao hilo tofauti na iliyotangazwa awali katika
mkutano mkuu wa makisio, huku wakisisitiza kuwa hawako tayari kuuza chini ya
bei ya awali.
Wakulima hao
walitoa msimamo huo jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi
wa habari, ambapo walisema katika mkutano huo walitangaziwa bei itakayotumika
kununulia kahawa katika msimu huu, na kuwa kwa sasa wanashangaa kuona wanapelekewa
barua ya kupunguzwa kwa bei hiyo.
Kwa
mujibu wa wakulima hao maandalizi ya
kahawa yanachukua muda mrefu ikia ni pamoja na kutumia gharama kubwa katika
kuandaa kahawa, huku wakiweka wazi msimamo wao wa kutokubaliana na sababu zozote
za kupunguza bei ya zao hilo, ambalo ndio tegemeo kwa wakulima wa mkoa wa
Kagera.
Mmoja wa
wakulima hao Bw. Burchard Laurent alisema kuwa bei iliyotangazwa awali ilikuwa nafuu kwa mkulima ambayo kwa kiasi fulani alidai
ingesaidia kuwapunguzia makali ya maisha yanayowakabili wakulima.
Alisema kauli
ya KCU ya kuwa tatizo hilo la kushusha bei linatokana na kushuka kwa bei ya
kahawa katika soko la dunia sio kweli kwani hata makapuni binafsi yanayonunua
kahawa ya wakulima kwa bei pia yangetangaza kushusha bei.
“Kama KCU
wataendelea kug’ang’ania kununua kahawa kwa bei ya punguzo wakulima hawatawauzia
kahawa yao na badala yake watawauzia wanunuzi na makampuni binafsi ambao mpaka
sasa wao bado wananunua kwa bei nzuri” alisisitiza Bw. Laurent
Awali KCU ilitangaza bei ya kununulia kahawa ya
wakulima ambapo kwa msimu wa 2012/2013 kahawa aina ya Robusta maganda
ilitangazwa kununuliwa kwa shilingi 1,360 kwa kilo huku Arabica maganda
ikitangazwa kununuliwa kwa shilingi 1,550.
Kwa
upande wa Robusta safi ilitangazwa
kununuliwa kwa shilingi 2,700 kwa kilo na shilingi 3,200 kwa
Arabica safi, huku kahawa ya Arabica organic iliyotangazwa ilikuwa
shilingi 3,800, Robusta ya Organic shilingi shilingi 3,650 na Robusta Organic
ya Uganda shilingi 1,700.
Hata hivyo Kwa
mujibu wa barua iliyoandikwa Juni 19 mwaka 2012 na kusainiwa na meneja mkuu wa KCU Bw. Vedasto Ngaiza na kusambazwa katika
vyama vyote vya ushirika vya msingi, bei ya kahawa inapungua tofauti na
iliyotangazwa awali kwa madai ya kushuka kwa bei ya zao hilo soko la
dunia.
Barua hiyo majiwa
imepata nakala inasema kahawa ya robusta ya maganda imepungua kutoka shilingi
1,360 hadi shilingi 1,100 kwa kilo moja, ambapo robusta safi imepungua kutoka
shilingi 2,700 hadi shilingi 2,200.
Aidha barua
hiyo inasema kuwa kahawa aina ya Arabica maganda imepungua kutoka shilingi 1,550
hadi shilingi 1,300 huku Arabica safi itapungua kutoka shilingi 3,200 awali hadi
shilingi 2,600.
Hata hivyo katika barua hiyo Meneja mkuu
huyo wa KCU Bw. Ngaiza anasema bei ya kahawa aina ya Robusta kwenye soko la
dunia ndio imeshuka, huku akiwa haonyeshi sababu za kupelekea KCU kushusha
kahawa aina ya Arabica .
mwisho
No comments:
Post a Comment