Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Saturday, March 24, 2012

Askari polisi auawa na kuporwa bunduki watu wasiofahamika


Na Mwandishi wetu
Bukoba
WATU wanaohofiwa kuwa majambazi wamemuua askari polisi mkoani Kagera PC Dickson (29) mwenye namba G 2626 na kisha kumpora bunduki aina ya SMG  na risasi 46, baada ya kumvamia akiwa kwenye lindo katika mgodi wa Turawaka wilayani Biharamulo mkoa wa Kagera.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Bw. Henry Salewi alisema kuwa askari huyo aliuawa jana, machi 23 ambapo mwili wake uligunduliwa saa 11 jioni na  askari wenzake  aliokuwa nao katika lindo mgodini hapo.

Bw. Salewi alisema kuwa PC Dickson aliuawa na watu wasiofahamika baada ya kupigwa kichwani mara nne kwa kutumia kifaa kinachotumika kuchimbia madini migodini, na kisha kupora bunduki hiyo iliyokuwa na risasi zake 46.

Alisema wakati wa tukio hilo jumla ya askari wanne walikuwa kwenye lindo katika mgodi huo wa kuchimba dhahabu wa Turawaka uliopo wilaya ya Biharamulo, ambapo walijipanga kuzunguka wa mgodi kutokana na kuwepo kwa vitendo vya watu kuutoboa kwenda kupora.

Kwa mujibu wa kamanda huyo baada ya askari aliokuwa nao kupita muda bila kumuona walianza kumtafuta na kumkuta amekwishauawa huku bunduki aliyokuwa nayo ikiwa haionekani.

Bw. Salewi alisema tayari mwili wa marehemu ulisafirishwa jana (Machi 24) kutoka mkoa wa Kagera kuelekea nyumbani kwao Sumbawanga kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Aidha kamanda huyo alisema jeshi la polisi tayari limeanza kufanya operasheni maalum ya kuwasaka wahusika wote katika mauaji ya askari huyo, ikiwa ni pamoja na kukamata bunduki iliyoporwa.

“Askari wote katika mgodi wa Turawaka na sehemu nyingine tayari wameingia porini kwa ajili ya msako mkali wa kuwakamata wahusika wote” alisema Kamanda huyo.
 Mwisho

No comments:

Post a Comment