Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Thursday, March 8, 2012

Wanachuo Bukoba waingizwa mkenge wadaiwa kutapeliwa milioni 27.4

Na Livinus Feruzi Bukoba.

JESHI la polisi mkoani Kagera linamshikilia mtu mmoja David Adongo kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, zaidi ya shilingi milioni 27.4.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Kagera Vitus Mlolere alisema kuwa juzi , polisi walipokea taarifa ya kwamba David amewatapeli wanachuo na kufanikiwa kumkamata.

Kamanda Mlolere alisema kuwa wanachuo wanaodai kutapeliwa ni 46, ambapo wanadai pamoja na chuo hicho kutosajiliwa pia hawafundishwi masomo waliyoahidiwa wakati wakijiunga na chuo mwaka jana.

 Alisema, chuo hicho kilichoko eneo la Miami Beach kata Kahororo katika manispaa ya Bukoba, kinadaiwa kuendesha shughuli zake kama tawi la chuo cha Victoria Institute of Tourism na Hotel Management cha jijini Mwanza.

Alisema, jeshi hilo limeanza uchunguzi kuhusiana na malalamiko hayo, na kuwa taarifa ya chuo hicho kama kimesajiliwa au la itatolewa baadae, baada ya kuwasiliana na chuo cha Victoria kilichoko Mwanza, ili tupate ukweli kama ni tawi lao au la.

 Baadhi ya wanachuo walisema kuwa, wana wasiwasi kama chuo hicho kimesajiliwa maana hata walipoelezwa kufanya mtihani wa taifa walidanganywa na kufanya mtihani ambao walidai aliutunga David mwenyewe, ambaye ni mkurugenzi wa chuo.

Annajoyce Josephat ambaye ni mwanachuo alisema kuwa wako wanachuo 50 wa kiume 21 na wa kike 29 na kuwa mwanzoni walikuwa wakipewa malazi na chakula, lakini baadae walitakiwa kujitegemea.

Naye Aneth Jerome alisema kuwa, awali waliahidiwa kusoma Utalii, Uhotelia na Uhasibu lakini baadae wakashangaa masomo hayo yanabadilika na kuambiwa pia watasoma Ualimu wa chekechea, Mistu na wanyama, Uandishi wa habari na Utawala.

Mwanachuo mwingine ni Helieth Henrico ambaye alidai wanalala katika mazingira hatarishi tofauti na walivyoahidiwa ambapo wamewekewa godoro chini na wanalala saba katika godoro moja.

“Wengine sio wakazi wa hapa (manispaa ya Bukoba) kuna waliotoka Karagwe, wapo wa Musoma mkoani Mara na maeneo mengine ya mkoani hapa na nje ya mkoa” alisema Helieth.

Wanachuo hao walidai kuwa wanalipa ada ya shilingi 850,000 kwa mwaka na kuwa kuna waliolipa ada ya mwaka mzima na baadhi yao wanalipa kwa awamu.
mwisho 

Ni sehemu ya mabweni ya chuo kilichopo mjini Bukoba, kinachodaiwa kuendesha shughuli zake kama tawi la chuo cha Victoria Institute of Tourism na Hotel Management cha jijini Mwanza wanafunzi wanadaiwa kulala kwenye godoro moja zaidi ya wanafunzi sita hadi saba.


NI Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw.Samwel Kamote akipata maelezo wanafunzi alipofika katika eneo la chuo hicho, hili ndio darasa linalotumiwa na wanafunzi hao

No comments:

Post a Comment