Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Wednesday, March 14, 2012

serikali yafunga chuo kilichowatapeli wanafunzi zaidi ya shilingi milioni 27.4

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Samwel Kamote akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya uamuzi wa kufunga chuo kinachodaiwa kuwa cha kitapeli

Na Livinus Feruzi
Bukoba.

MKUU wa wilaya ya Bukoba Bw. Samwel Kamote ameagiza kufungwa kwa chuo kilichopo mjini Bukoba kinachodaiwa kuwa tawi la chuo cha Victoria Institute of Tourism and Hotel management kilichoko jijini Mwanza, kwa madai kuwa ni cha kitapeli na hakina vigezo vya kuitwa chuo.

Hatua ya kufunga chuo hicho imefikiwa baada ya mkuu huyo wa wilaya ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchuo, ambapo aliamua kwenda kujionea hali halisi na kupata taarifa ya chuo, kilichoko eneo la Miami Beach kata Kahororo katika manispaa ya Bukoba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Bw. Kamote alisema mazingira ya chuo ni ya kusikitisha hasa sehemu wanapolala, ambapo  magodoro yamechoka, yamewekwa chini na chumba kimoja kidogo, huku pia watoto wengi wakilala katika godoro moja.

Alisema utaratibu wa serikali lazima vyuo vyote visajiliwe na mamlaka zinazohusika lakini chuo kinachodaiwa kuwa cha kitapeli kinaendesha shughuli zake bila usajili.

Bw. Kamote alisema kinachoshangaza zaidi na kuona chuo kimoja kinatoa masomo ambayo ni mchanganyiko ikiwa ni pamoja na masomo ya walimu wa shule za chekechea, mistu na hifadhi ya wanyama pori, utalii na uhotelia, uandishi wa habari, uhasibu na utawala.

“Hata mchanganyiko na mjumuiko wa masomo ulivyo tu ni feki na ni wa kitapeli, na nimeagiza wanafunzi wote kurudi nyumbani, wakati huo mhusika pamoja na kuwarejeshea wazazi fedha zao, atatakiwa kuwatafutia vyuo sahihi ili waendelee na masomo yao na kufanya mtihani” alisema Bw. Kamote.

Bw. Kamote alisema kuwa, kutokana na kuwepo kwa tetesi za vyuo vingi vya namna hiyo katika wilaya yake, amemwagiza mkurugenzi wa manispaa kupitia kwa afisa elimu kufanya ukaguzi katika vyuo vyote ili kuona kama vina usajili na vinatoa masomo gani.

Alisema kuwa ameagiza baada ya ukaguzi vyuo vitakavyobainika ni vya kitapeli vifungwe na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wamiliki kama ilivyofanyika kwa  Bw. David Adongo ambaye ndiye mmiliki wa chuo kilichofungwa.

Hata hivyo Bw. Kamote aliwataka wazazi na walezi, kuwa waangalifu kabla ya kuwapeleka watoto wao kujiunga na vyuo, ili kuepuka kukumbwa na utapeli wa namna hiyo, kutokana na kudaiwa kuongezeka kwa vyuo vya kutapeli.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kagera Bw. Vitus Mlolere alisema alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa hakuna uhusiano baina ya  mmiliki wa chuo hicho cha amjini Bukoba  na Chuo cha Victoria institute of tourism and hotel management cha jijini Mwanza.

Aidha alisema  chuo hicho tayari kilishatembelewa na mkaguzi wa shule wa manispaa na kumwandikia mmiliki barua ya kukifunga, lakini alikaidi agizo hilo na hivyo kuendelea kufanya kazi hiyo kinyume cha sheria.

Kamanda Mlolere alisema kuwa Machi 6 mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wanachuo kuwa wametapeliwa na kufanikiwa kumkamata mkurugenzi huyo kwa tuhuma za kujipatia fedha zaidi ya shilingi milioni 27.4 kwa njia ya udanganyifu.

Baaadhi ya wanachuo ambao wanadai kutapeliwa walisema baadhi yao walilipa ada ya shilingi 850,000 kwa mwaka, wako 50 wa kike 29 na wakiume 21, na kuwa wamekuwa wakilala saba katika godoro moja ambalo limewekwa chini kutona na sehemu wanakolala kutokuwa na vitanda.

Kwa mujibu wa Kamote chuo hicho kilikuwa na walimu tisa ambao walikimbia baada ya mmiliki kukamatwa na polisi.


Mwisho.


No comments:

Post a Comment