Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Saturday, March 10, 2012

Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yanaathiri Tanzania katika kudumisha utawala bora nchini

Na Livinus Feruzi
 Bukoba

 MAUAJI ya walemavu wa ngozi (albino), vikongwe na vitendo vya ubakaji na ukatili majumbani, vimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri juhudi za serikali ya Tanzania katika kudumisha utawala bora.

 Katibu tawala wa mkoa wa Kagera Bw. Nassor Mnambila alisema hayo jana mjini Bukoba kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Kanali mstaafu Fabiani Massawe wakati akifungua mkutano mkuu wa tathimini ya utawala bora uliowakutanisha wadau  timu ya wataalamu wa mpango wa tathimini ya utendaji kwa nchi za Afrika (APRM).

Alisema Tanzania ni nchi inayozingatia msingi ya utawala bora na demokrasia, ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binadamu , ambapo alisema siku za karibuni suala la utawala bora limekuwa na msisitizo na kupewa umuhimu wa kipekee.

 Bw. Mnambila alisema juhudi za serikali za kudumisha utawala bora zinaenda sambamba na ushirikishwaji wa wananchi katika kufanya maamuzi yanayohusu masuala mbalimbali ili kuwezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uwazi zaidi.

Kutokana na hali hiyo alisema kila mwananchi anatakiwa kupiga vita vitendo hivyo ambavyo vinaonekana kutia doa serikali ya tawananchi ni bora.

 Mwenyekiti wa chama cha walemavu wa ngozi (Albino) Bw. Buchard Mpaka alisema kuwa tangu kuibuka kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi mwaka 2008, kwa mkoa wa Kagera mpaka sasa jumla ya albino saba waliuawa na watu wasiofahamika kwa imani za kishirikina.

 Alisema mbali na kuuawa kwa watu hao wasio na hatia, pia albino kadhaa walikatwa viungo mbalimbali na hivyo kuachwa na ulemavu wa kudumu, huku wakikimbia na kuacha makazi yao.

Naye Bi. Hilde Festo kutoka chama cha viziwi (CHAVITA) tawi la mkoa wa Kagera alisema viziwi wanakosa huduma muhimu za matibabu kwenye hospitali na ofisi nyingine za umma kutokana kutokuwepo watu wa kutafusiri lugha ya ishara (wakalimani).

 “Ukosefu wa wakalimani wa lugha za alama ni tatizo kubwa kwa viziwi, hata kwenye ofisi za umma wanashindwa kueleza shida zao ili kuzipatia ufumbuzi kwa sababu hakuna wataalamu wa kutafasiri lugha za ishara” alisema Bi. Festo.

Aidha walemavu hao walilalamikia ukosefu wa shule maalumu za walemavu na mazingira yasiyo rafiki kwao na kuwa hatua hiyo inasababisha walemavu kukosa haki za msingi hivyo kukwamisha juhudi za utawala bora nchini.

 Mwisho
Kiongozi wa ujumbe kutoka nje ya nchi Profesa Adel Janade wa Nigeria akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa kutathimini utawala bora, mkutano huo ulifanyika katika manispaa ya Bukoba, ambapo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa wilaya zote za mkoa wa Kagera.
Washiriki wa mkutano wa kutathimini utawala bora wakifuatilia masuala mbalimbali yanayohusu utawala bora nchini Tanzania
Katibu tawala wa mkoa wa Kagera Bw. Nassor Mnambila akifungua mkutano mkuu wa kutathimini  utawala bora kwa  niaba ya mkuu wa mkoa wa Kageru , mkutano huo uliwakutanisha wadau na  timu ya wataalamu wa mpango wa tathimini ya utendaji kwa nchi za Afrika (APRM).

No comments:

Post a Comment