Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Monday, March 19, 2012

Nyavu zenye thamani ya zaidi ya Bilioni 1.5 zateketezwa Kagera

Sehemu ya nyavu haramu za uvuvi zilizokamatwa na waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt. Mathayo Devid Mathayo katika mwalo wa Ibagiro Bukoba vijijini na kisha kuziteketeza kwa moto.
Ni rundo la nyavu haramu zilizokamatwa katika mwalo wa Igabiro zikisubiri kuteketezwa kwa moto, nyavu hizi zilikamatwa baada ya ziara ya kushtukiza.
Mzee huyu anafuatilia  jinsi nyavu haramu zinavyoteketea  kwa moto, ingawa kuna jua kali lakini anajikinga kwa koti ili ziteketee akiziona kwa macho yake.
Vijana wa kazi hata nao wapo kwa ajili ya kuangalia usalama kweli wamejiandaa kukabiliana na lolote linaloweza kutokea.
Baada ya kazi ngumu sasa ni kurejea tulikotokea kazi ilikuwa ngumu  ni Waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt. Mathayo Devid kulia mwenye suti na mkuu wa mkoa wa Kagera aliyevaa kofia wakipanda mlima ulipo mwalo wa Igabiro baada kukamata nyavu takribani 1000 na kisha kuziteketeza kwa moto.Na Livinus Feruzi
Bukoba.

WAZIRI wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt. Mathayo Devid Mathayo jana ameteketeza nyavu za uvuvi  haramu zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5, ambazo zilifanikiwa kukamatwa katika kipindi cha miaka mwili iliyopita zikitumika katika shughuli za uvuvi kinyume cha sheria.

Zoezi la kuteketeza nyavu hizo haramu lilifanyika katika eneo la Kyakailabwa manispaa ya Bukoba, na kushirikisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa uvuvi nchini Bw. Hoseah Mbilinyi na mkuu wa mkoa wa Kagera Bw. Fabian Massawe.

Awali Ofisa mfawidhi wa kikosi cha ulinzi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi kanda ya Kagera, Bw. Rodrick Mahimbali alisema vyavu  hizo zilikamatwa kwa kipindi cha mwaka 2009/10 na mwaka 2010/2011.

Bw. Mahimbali alitaja zana hizo kuwa ni pamoja na kokoro 503, timba 785, makila 12,965, nyavu za dagaa na kamba za kuvutia kokoro zenye urefu wa mita 192,274, ambapo alisema kukamatwa kwa zana hizo kulitokana na ushirikiano baina ya kikosi hicho na wadau mbalimbali.

Alisema nyavu  hizo zilikamatwa kwenye mialo mbalimbali ya ziwa Victoria, vituo vya mabasi, maghala, vyombo vya uvuvi na katika makazi ya wananchi na kuwa baada ya kukamatwa zilihifadhiwa katika ofisi ya doria zikisubiri kuteketezwa.

“Kwa miaka miwili iliyopita kikosi cha ulinzi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi kanda ya Kagera zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 na kuzihifadhi zikisubiri kuteketezwa mheshimiwa waziri tunaomba siku ya leo uteketeze nyavu hizi” alisema Bw. Mahimbali.

Mbali na kuteketezwa nyavu hizo zilizokamatwa na kikosi cha doria pia Waziri Mathayo juzi aliteketeza vyavu zinazokadiriwa kufikia 1,000 ambazo alizikamata mwenyewe wakati wa ziara ya kushtukiza katika mwalo wa Igabiro uliopo Bukoba vijijini.

Hata hivyo pamoja na mambo mengine Dkt. Mathayo aliwataka wavuvi nchini kutambua madhara ya uvuvi haramu huku wakiwatahadharisha kuwa wasipoacha uvuvi haramu kuna hatari ya samaki katika ziwa Victoria kubaki historia ikiwemo wananchi kukosa kipato.

Mwisho


No comments:

Post a Comment