Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Friday, March 2, 2012

mabadiliko ya tabia nchi


Na Mwandishi wetu

MABADILIKO ya tabia nchi nchini Tanzania yameathiri sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo ukosefu wa umeme wa uhakika na mafuriko hali inayohitaji nguvu za pamoja ili kuokoa maisha ya watanzania na dunia kwa ujumla.


Mkurugenzi mtendaji wa nchi za Afrika juu ya mabadiliko ya tabia nchi (APCCC) Bw. Edward Munaaba alisema hayo mjini Bukoba wakati wa mkutano wa asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na mabadiliko ya tabia nchi kutoka mikoa mitano.


Mkutano huo ulilenga kukusanya maoni juu ya mkakati wa taifa wa mabadiliko ya tabia nchi, ambapo ulizishirikisha asasi mbalimbali kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kigoma na Kagera.


Bw. Munaaba alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, takribani wizara zote za serikali zimeathirika na kupelekea wananchi na jamii kwa ujumla wakiwemo wanyama na mimea kupata madhara makubwa.


Akitolea mfano katika wizara ya nishati na madini alisema tatizo la kukosekana kwa umeme wa kutosha hapa nchini kwa siku za karibuni limesababishwa na kupungua kwa maji katika mabwawa ya kuzalishia nishati hiyo ya umeme.


Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo utafiti uliofanywa na jukwaa la asasi zisizo za serikali zinazojihusisha na mabadiliko ya tabia nchi ulibaini kuwa kina cha maji katika ziwa Victoria kimepungua kwa kiasi kikubwa, huku tatizo hilo likiathiri zaidi sekta ya uvuvi.


Alisema ni bora kila mwananchi nchini kutambua hadhari za mabadiliko ya tabia nchi na kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo kunusuru uchumi wa taifa na maisha ya wananchi na viumbe vingine.

Wakitoa maoni juu ya mkakati huo wadau wa mazingira walisema inatakiwa kila sekta kuweka tahadhari mapema juu dhana ya mabadiliko ya tabia nchi katika mipango yote ya maendeleo kutokana na kile walichodai kuwa dhana hiyo bado haijapewa kipaumbele.

  
Walisema umaskini wa kipato kwa watanzania wengi ndio unasababisha huaribifu wa mazingira, ambapo walisema asilimia kubwa ya wananchi wanaedelea kukata miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali kutokana na kukusa fedha za kutumia nishati mbadala wakitoa mfano nishati ya jua na upepo. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment