Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Wednesday, March 21, 2012

Wachimbaji wa dhahabu chato waua wenzao wawili na kisha kuwachoma moto

Kamanda wa Jeshi la Polisi wa mkoa wa Kagera Bw. Henry Salewi aliyenyosha kidole akiongea na waendesha pikipiki zinazofanya kazi ya kubeba abiria mjini Bukoba, pembeni mwake ni Kamanda wa kikosi cha usalama mkoa huo Bw. Marson Mwakyoma( picha kwa hisani ya mtandao.
Na Mwandishi wetu
Bukoba

WACHIMBAJI wadogo wawili katika machimbo ya Matabe yaliyoko wilaya ya Chato mkoa mpya wa Geita wamefariki dunia, baada ya kupigwa na wachimbaji wenzao na kisha kuwachoma moto kwa kuwatuhumu kujihusisha na vitendo vya wizi.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera aliwataja waliouawa kuwa ni Jumanne William (35) na Juma Magese (40) wote wachimbaji wa wadogo wadogo wa dhahabu.

Alisema wachimbaji hao waliuawa mwishoni mwa wiki saa 11 jioni baada ya kukamatwa wakiwa na jaketi inayodaiwa kuibiwa wakati wa tukio la wizi lililofanyika mwezi mmoja uliopita, ambapo wachimbaji hao walivamiwa na kuporwa dhahabu.
 
Kamanda Salewi aliongeza kuwa siku ya tukio Jumanne William (35) alikamatwa na wachimbaji wenzake akiwa na jaketi linalodaiwa kuibiwa mwezi Februari mwaka huu katika tukio la wizi lililotokea machimboni hapo.
 
Kwa mujibu wa Kamanda Salewi baada ya William kuhojiwa alimtaja mchimbaji mwenzake Juma Magese kuwa ndiye aliyempatia jaketi hilo na kumtaka awapeleke kwake, na kuwa walipofika alikiri kuhusika katika tukio la mwezi Februari ndipo watuhumiwa hao walianza kupigwa hadi kufa na kisha kuwachoma moto.
 
Alisema polisi inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika, ambapo alisema polisi wanaendelea kuwahoji ili kubaini wahusika wote katika mauaji hayo.
 
Wakati huo huo alisema polisi inawashikilia watu wawili wanasadikiwa kuwa majambazi katika wilaya ya Karagwe,ambao walikamatwa wakitaka kuvamia kituo cha mafuta cha Mkakarongo kilichopo wilayani humo kwa ajili ya kupora fedha.
 
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Apoli John (33) na Mushabe John (25) ambao alisema baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa wakiwa na bastola moja aina ya (smoke) ambayo inadaiwa haikuwa na risasi.
 
 
Kamanda Salewi alisema polisi walipata taarifa za majambazi hao na kuweka mtego ambao ulifanikisha kuwakamata kabla ya kutekeleza ujambazi huo.
 
Mwisho    


No comments:

Post a Comment