Na Mwandishi
wetu
Bukoba
WATU
wanaohofiwa kuwa majambazi wamemuua askari polisi mkoani Kagera PC Dickson (29)
mwenye namba G 2626 na kisha kumpora bunduki aina ya SMG na risasi 46,
baada ya kumvamia akiwa kwenye lindo katika mgodi wa Turawaka wilayani
Biharamulo mkoa wa Kagera.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Kagera Bw. Henry Salewi alisema kuwa askari huyo aliuawa jana,
machi 23 ambapo mwili wake uligunduliwa saa 11 jioni na askari wenzake
aliokuwa nao katika lindo mgodini hapo.
Bw. Salewi
alisema kuwa PC Dickson aliuawa na watu wasiofahamika baada ya kupigwa kichwani
mara nne kwa kutumia kifaa kinachotumika kuchimbia madini migodini, na kisha
kupora bunduki hiyo iliyokuwa na risasi zake 46.
Alisema wakati
wa tukio hilo jumla ya askari wanne walikuwa kwenye lindo katika mgodi huo wa
kuchimba dhahabu wa Turawaka uliopo wilaya ya Biharamulo, ambapo walijipanga
kuzunguka wa mgodi kutokana na kuwepo kwa vitendo vya watu kuutoboa kwenda
kupora.
Kwa mujibu wa
kamanda huyo baada ya askari aliokuwa nao kupita muda bila kumuona walianza
kumtafuta na kumkuta amekwishauawa huku bunduki aliyokuwa nayo ikiwa
haionekani.
Bw. Salewi
alisema tayari mwili wa marehemu ulisafirishwa jana (Machi 24) kutoka mkoa wa
Kagera kuelekea nyumbani kwao Sumbawanga kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Aidha kamanda
huyo alisema jeshi la polisi tayari limeanza kufanya operasheni maalum ya
kuwasaka wahusika wote katika mauaji ya askari huyo, ikiwa ni pamoja na
kukamata bunduki iliyoporwa.
“Askari wote
katika mgodi wa Turawaka na sehemu nyingine tayari wameingia porini kwa ajili
ya msako mkali wa kuwakamata wahusika wote” alisema Kamanda huyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment