Na Mwandishi wetu
Bukoba
WACHIMBAJI wadogo wawili katika machimbo ya Matabe
yaliyoko wilaya ya Chato mkoa mpya wa Geita wamefariki dunia, baada ya kupigwa
na wachimbaji wenzao na kisha kuwachoma moto kwa kuwatuhumu kujihusisha na
vitendo vya wizi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera aliwataja waliouawa
kuwa ni Jumanne William (35) na Juma Magese (40) wote wachimbaji wa wadogo
wadogo wa dhahabu.
Alisema wachimbaji hao waliuawa mwishoni mwa wiki saa
11 jioni baada ya kukamatwa wakiwa na jaketi inayodaiwa kuibiwa wakati wa tukio
la wizi lililofanyika mwezi mmoja uliopita, ambapo wachimbaji hao walivamiwa na
kuporwa dhahabu.
Kamanda Salewi aliongeza kuwa siku ya tukio Jumanne
William (35) alikamatwa na wachimbaji wenzake akiwa na jaketi linalodaiwa kuibiwa
mwezi Februari mwaka huu katika tukio la wizi lililotokea machimboni hapo.
Kwa mujibu wa Kamanda Salewi baada ya William kuhojiwa
alimtaja mchimbaji mwenzake Juma Magese kuwa ndiye aliyempatia jaketi hilo na
kumtaka awapeleke kwake, na kuwa walipofika alikiri kuhusika katika tukio la
mwezi Februari ndipo watuhumiwa hao walianza kupigwa hadi kufa na kisha
kuwachoma moto.
Alisema polisi inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za
kuhusika, ambapo alisema polisi wanaendelea kuwahoji ili kubaini wahusika wote
katika mauaji hayo.
Wakati huo huo alisema polisi inawashikilia watu
wawili wanasadikiwa kuwa majambazi katika wilaya ya Karagwe,ambao walikamatwa
wakitaka kuvamia kituo cha mafuta cha Mkakarongo kilichopo wilayani humo kwa
ajili ya kupora fedha.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Apoli John (33) na
Mushabe John (25) ambao alisema baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa
wakiwa na bastola moja aina ya (smoke) ambayo inadaiwa haikuwa na risasi.
Kamanda Salewi alisema polisi walipata taarifa za
majambazi hao na kuweka mtego ambao ulifanikisha kuwakamata kabla ya kutekeleza
ujambazi huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment