Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Friday, March 16, 2012

serikali yashtuka kutoka usingizini yaanza kuhaha kunusuru uwanja wa Kaitaba


Na Livinus Feruzi
Bukoba

BAADA ya muda mrefu wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba kudaiwa kupoteza mapato yanayotokana na uwanja wa mpira wa miguu wa Kaitaba katika shughuli nje ya mpira, hatimaye halmashauri hiyo imeshtuka kutoka usingizini na kuamua kuweka mwongozo wa kusimamia utumiaji wa uwanja huo.

Kupotea kwa mapato hayo kunaelezwa kuchangia halmashauri hiyo kushindwa kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara uwanja huo ikiwemo kutomaliza deni la shilingi milioni 53 wanazodai timu ya Kagera sukari walizotumia wakati wa kuutengeneza.

Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Bw. Robart Kwela alisema
baada ya kubaini kwamba shughuli nyingi zinazofanyika ndani ya uwanja tofauti na mpira zinaingizia halmashauri fedha kidogo, huku waandaaji wa shughuli hizo wakinufaika zaidi, wameamua kuweka mwongozo maalum.

Alisema kamati ya fedha (CMT) iliyokuta mwezi uliopita wameamua kuweka utaratibu kuwa shughuli yoyote itakayofanyika ndani ya uwanja tofauti na mpira itatakiwa kulipia shilingi milioni moja tofauti na utaratibu uliokuwepo.

Bw. Kwela alisema awali matumizi ya uwanja huo yalikuwa hayaeleweki kutokana na kile kinachoelezwa kuwa, watu wamekuwa wakikusanya fedha nyingi katika maonyesho mbalimbali lakini halmashauri imekuwa ikiambulia fedha kiduchu.

“Kiukweli shughuli nyingine zinaingizia halmashauri fedha kidogo, lakini CMT tumeishaliona na tayari tumeweka mwongozo chini ya milioni moja hakuna atakayeruhusiwa kutumia uwanja huu” alisema Kaimu mkurugenzi huyo.

Alisema mwongozo huo utasaidia halmashauri kupata fedha, ambazo zitakuwa zikitumika kufanya marekebisho ya mara kwa mara, katika uwanja huo ili  kuondoa mapungufu yanayakabili uwanja wa Kaitaba wakati wakijiandaa kuweka sheria za kuusimamia.

Akizungumzia deni la timu ya Kagera sukari la milioni 53, Bw. Kwela alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Agosti mwaka jana halmashauri bado ilikuwa inadaiwa na timu hiyo zaidi ya shilingi milioni 11.4.

Kuhusu agizo la TFF la kuufanyia marekebisho uwanja huo, alisema baadhi ya mapungufu tayari yamefanyiwa kazi, ambapo uzio wa kutenganisha wachezaji na watazamaji na sehemu ya kuchezea (pitch) vimerekebishwa.

Bw. Kwela alisema halmashauri imepanga kuendelea kuufanyia marekebisho uwanja huo kulingana na ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza kero zinazoukabili.

Hata hivyo hivi karibuni Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania
(TFF ) walitishia kufunga uwanja huo kutotumiwa na timu ya Kagera sugar kama uwanja wa nyumbani, katika mchezo wa ligi kuu ya vodacom kwa madai ya kutokidhi viwango na vigezo vya kiusalama.

Miongoni mwa matatizo yanayokabili uwanja huo ambayo TFF iliagiza kuyafanyia marekebisho ni pamoja na ukosefu wa maji baada ya kukatiwa huduma hiyo kwa kushindwa kulipa deni la milioni mbili na hivyo kufanya vyoo kutotumika na kuharibika kwa mbao sehemu ya kukaa watazamaji.

Mwisho



Mwonekano wa uwanja wa mpira wa miguu wa Kaibata katika sehemu ya kuchezea mpira (pitch)
  
Mwonekano wa jukwaa dogo la watazamaji ambalo  hata hivyo mbao zinaonekana kuharibika

No comments:

Post a Comment