Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Samwel Kamote akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya uamuzi wa kufunga chuo kinachodaiwa kuwa cha kitapeli |
Na
Livinus Feruzi
Bukoba.
MKUU wa wilaya ya Bukoba Bw. Samwel
Kamote ameagiza kufungwa kwa chuo kilichopo mjini Bukoba kinachodaiwa kuwa tawi
la chuo cha Victoria Institute of Tourism and Hotel management kilichoko jijini
Mwanza, kwa madai kuwa ni cha kitapeli na hakina vigezo vya kuitwa chuo.
Hatua ya kufunga chuo hicho imefikiwa
baada ya mkuu huyo wa wilaya ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchuo, ambapo
aliamua kwenda kujionea hali halisi na kupata taarifa ya chuo, kilichoko eneo
la Miami Beach kata Kahororo katika manispaa ya Bukoba.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Bw. Kamote alisema mazingira ya chuo ni ya kusikitisha hasa
sehemu wanapolala, ambapo magodoro
yamechoka, yamewekwa chini na chumba kimoja kidogo, huku pia watoto wengi wakilala
katika godoro moja.
Alisema utaratibu wa serikali lazima
vyuo vyote visajiliwe na mamlaka zinazohusika lakini chuo kinachodaiwa kuwa cha
kitapeli kinaendesha shughuli zake bila usajili.
Bw. Kamote alisema kinachoshangaza
zaidi na kuona chuo kimoja kinatoa masomo ambayo ni mchanganyiko ikiwa ni
pamoja na masomo ya walimu wa shule za chekechea, mistu na hifadhi ya wanyama
pori, utalii na uhotelia, uandishi wa habari, uhasibu na utawala.
“Hata mchanganyiko na mjumuiko wa
masomo ulivyo tu ni feki na ni wa kitapeli, na nimeagiza wanafunzi wote kurudi
nyumbani, wakati huo mhusika pamoja na kuwarejeshea wazazi fedha zao, atatakiwa
kuwatafutia vyuo sahihi ili waendelee na masomo yao na kufanya mtihani” alisema
Bw. Kamote.
Bw. Kamote alisema kuwa, kutokana na
kuwepo kwa tetesi za vyuo vingi vya namna hiyo katika wilaya yake, amemwagiza mkurugenzi
wa manispaa kupitia kwa afisa elimu kufanya ukaguzi katika vyuo vyote ili kuona
kama vina usajili na vinatoa masomo gani.
Alisema kuwa ameagiza baada ya ukaguzi
vyuo vitakavyobainika ni vya kitapeli vifungwe na hatua za kisheria zichukuliwe
kwa wamiliki kama ilivyofanyika kwa Bw.
David Adongo ambaye ndiye mmiliki wa chuo kilichofungwa.
Hata hivyo Bw. Kamote aliwataka
wazazi na walezi, kuwa waangalifu kabla ya kuwapeleka watoto wao kujiunga na
vyuo, ili kuepuka kukumbwa na utapeli wa namna hiyo, kutokana na kudaiwa
kuongezeka kwa vyuo vya kutapeli.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kagera
Bw. Vitus Mlolere alisema alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa hakuna
uhusiano baina ya mmiliki wa chuo hicho cha
amjini Bukoba na Chuo cha Victoria
institute of tourism and hotel management cha jijini Mwanza.
Aidha alisema chuo hicho tayari kilishatembelewa na mkaguzi
wa shule wa manispaa na kumwandikia mmiliki barua ya kukifunga, lakini alikaidi
agizo hilo na hivyo kuendelea kufanya kazi hiyo kinyume cha sheria.
Kamanda Mlolere alisema kuwa Machi 6
mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wanachuo kuwa wametapeliwa na
kufanikiwa kumkamata mkurugenzi huyo kwa tuhuma za kujipatia fedha zaidi ya
shilingi milioni 27.4 kwa njia ya udanganyifu.
Baaadhi ya wanachuo ambao wanadai
kutapeliwa walisema baadhi yao walilipa ada ya shilingi 850,000 kwa mwaka, wako
50 wa kike 29 na wakiume 21, na kuwa wamekuwa wakilala saba katika godoro moja
ambalo limewekwa chini kutona na sehemu wanakolala kutokuwa na vitanda.
Kwa mujibu wa Kamote chuo hicho
kilikuwa na walimu tisa ambao walikimbia baada ya mmiliki kukamatwa na polisi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment