Matangazo yanakaribishwa katika blog hii,piga simu no 0753 239 687 Email-livinusferuzi@yahoo.com

Wednesday, May 22, 2013

KIGOGO WA HALMASHAURI APANDISHWA KIZIMBANI



 
Mkurugenzi wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini Dkt Edward Hoseah


Na Mwandishi wetu
Bukoba.

KAIMU afisa ushirika wa wilaya ya Missenyi Faustina Majala amefikishwa mahakamani na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoa wa Kagera akikabiliwa na mashtaka kumi.

Makosa yanayomkabili afisa huo ni pamoja na kupokea rushwa na kughushi nyaraka, ambapo inadaiwa alitenda makosa hayo kati ya Mei 26 mwaka 2007 hadi Mei 27 mwaka 2008.

Akisomewa mashtaka mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bukoba Sylivia Lushasi na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Ronald Manyiri alisema mshitakiwa alitenda makosa hayo akiwa na nafasi mbalimbali za uongozi.

Manyiri alisema mshitakiwa huyo akiwa kaimu afisa ushirika wa wilaya ya Bukoba, mkuu wa vyama vya ushirika vya msingi wilaya hiyo na mjumbe wa mkutano mkuu wa chama kikuu cha ushirika ushirika mkoa wa Kagera KCU(1990) Ltd alifanya makosa matatu ya kughushi nyaraka kinyume cha sheria.

Aidha anashtakiwa kwa makosa matatu ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri na mengine matatu ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha shilingi 340,000,  huku katika shtaka la kumi mshitakiwa anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake.

Mshitakiwa amekana makosa hayo na yuko nje kwa dhamana hadi  Juni 5 mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa tena.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment